Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu katika kipengele chetu cha ''KWA TAARIFA YAKO'' ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui pia yawezekana ilitukia ukawa unaijua lakini GK ikawa imesahau mahali au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuweka comment yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu.
Zawadi Machibya akiuliza swali kwa waziri mkuu mh. Mizengo Pinda (hayupo pichani) alipotembelea nchini Uingereza mwaka jana.
Katika KWA TAARIFA YAKO hii leo tuko na mtangazaji maarufu nchini na ukanda wa Afrika mashariki . Huyu si mwingine bali ni Zawadi Machibya, mtangazaji wa Shirika la utangazaji la Uingereza BBC tokea mwaka 2009 mpaka hivi sasa (vijana wa sasa wanasema Jembe), akisikika kupitia idhaa ya Kiswahili ya shirika hilo. Awali alikuwa mwajiriwa wa Shirika la utangazaji Tanzania toka mwaka 1994 hadi 2000 akianzia Radio Tanzania, enzi hizo ikiitwa (RTD), kisha kuanzia mwaka 2000 hadi 2008 kwenye runinga ikiitwa TVT, kabla haijabadilishwa kuwa TBC ambako amefanya vipindi mbalimbali kama vya Mahojiano, Tuambie, mijadala, vipindi vya wanawake na watoto, Bunge, vipindi vingine vikiwemo kuripoti matukio, kuandika makala na kadhalika.
Milton na Gift watoto wa Zawadi katika pozi.
Zawadi, mama wa familia ya watoto watatu, Milton, Gift na Godson ana mengi ambayo jamii haiyajui labda kwa watu wake wa karibu. sasa KWA TAARIFA YAKO Zawadi ndiye aliyeweka rekodi nchini kwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke katika serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu nchini akiwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino Mwanza (SAUT) Pia ni mmoja wa waanzilishi wa umoja wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu (TAHLISO). Licha ya hayo, Zawadi ameokoka na anampenda Yesu, akiwa pia amefanya huduma mbalimbali vijijini kabla ya kuingia ulimwengu wa habari, lakini ilikuwaje mpaka akaamua kuingia kwenye media?
"Niliipenda kazi hii tangu mtoto. Nilipenda lugha hata kusomea masomo ya (HGL), na kuwapasha watu habari, matukio, kuwapa taarifa. Nimemaliza shule, JKT( ambako akiwa mafunzoni alikuwa mchungaji akisaidiana na mwenzake anayefahamika kwa jina la Busara).Halafu nikaanza kazi ya Injili vijijini (Singida) semina, mikutano ya nje uimbaji (Huduma Band na akina Pastor Abel Orgenes, Grace Msusu, Magreth, Elia Kisigila, Elisante,Arthur na wengine.) Muda umefika natakiwa chuo, lakini naona tangazo la kazi Daily News-kwa Radio Tanzania, SHIHATA, Idara ya Habari Maelezo. Nika-apply lakini kwakuifanyia maombi mazito barua yangu ya kuombea kazi, nikaziombea barua, nikazituma. Halafu nikaendelea na huduma, wakati Fernandus Venon na huduma ya SOM-School of Ministry ya Morris Cerullo, wakija Singida, nikafanya kazi. Baadaye napokea barua ya kuitwa kwenye usaili na kisha kupata kazi radio Tanzania nikiwa MADHABAHUNI" amebainisha Zawadi.
Watoto wa zawadi, Gift pamoja na Godson.
Lakini vipi kuhusu wokovu na kazi yake anasemaje ''Inatangulia IMANI, ndiyo inanifanya hivi nilivyo. Kuna mamlaka iliyo kuu, ambayo inasimamia na kuongoza kila ninachofanya. Naamini uzima unaanzia rohoni, halafu unashuka kwenye nafsi halafu mwilini. Kama roho haina uongozi HASA WA KIMUNGU, ni vigumu kuvuka majaribu, changamoto, majukumu, na ufahamu -(Knowledge) Chanzo ni kumcha Mungu). Pili, macho ya rohoni. Giza duniani kubwa bila msaada wa macho ya rohoni, si rahisi kuona''.
Zawadi akimwelekeza kitu bwana Julius Malema mwanasiasa kijana maarufu wa Afrika ya kusini alipofika ofisi za BBC London mapema mwaka jana.
"Utakumbuka kuwa Yesu aliwaonya watu juu ya ‘kuwa macho na waandishi wa habari na …..wengineo.’ La msingi ni kuwa uandishi na utangazaji ni kazi ya watu. Unawapa nini, unatangaza nini na je WEWE UNAJUA NINI KUHUSU WATU NA MAISHA YAO KISIASA, KIJAMII, KIUCHUMI, KIMAISHA, UTAMADUNI WAO, IMANI ZAO, n.k.Na unapofika ngazi ya kimataifa kama hivi hii ya BBC, wigo wako kiuelewa lazima uendane na hadhi ya chombo unachokitumikia. Mfano kujua nani anafanya nini wakati gani, kwa manufaa ya nani na kwa kiwango gani na mengine mengi! Hapa utaleta mataifa makubwa ya Ulaya, Marekani, China, Afrika kama Bara, viongozi wake na bila kusahau majanga yanayoikumba dunia likiwemo ‘kudorora kwa uchumi na mzozo kuhusu sarafu ya Euro’ utaona kuwa maeneo mengine kama yanaoendelea huko Australia, hali ikoje na mengine". amesema Zawadi.
KWA TAARIFA YAKO kuna watu mbalimbali ambao wamechangia mafanikio yake katika ulimwengu wa habari, ambapo ameiambia GK kuwa ''Kwa upande wa kazi, ni mzoefu na mwalimu mzuri. Niko kwenye taaluma hii kwa karibu miaka ishirini sasa. Watu wa muhimu kuwakumbuka hapa ni Mama Edda Sanga ndiye aliyenifundisha kazi (RTD), lakini na wengine wazoefu wakiwemo.
Unaweza kumsikia Zawadi vyema kupitia vipindi vya Dira ya dunia, Leo Afrika na vinginevyo kupitia Idhaa ya Kiswahili ya BBC ikikutangazia moja kwa moja kutoka jijini London nchini Uingereza. Zawadi anayo mengi ya kueleza, GK itamtafuta tena kwa maongezi zaidi.
Zawadi Machibya pamoja na John Solombi (ndani ya studio) wakiwa katika moja ya studio zilizokuwa katika jengo la zamani la BBC, Bush House jijini London, hapa ni kipindi cha ''Dira ya dunia''
Zawadi mkono wa kushoto akiwa na John Solombi katika Dira ya dunia.
Zawadi akiwajibika kumtumikia Mungu katika moja ya mikutano vijijini.
Zawadi enzi hizo akiwa katika huduma moja ya kijiji mkoani Morogoro.
Zawadi akiwa pamoja na mumewe Apostle Machibya. picha ya enzi hizo.
Haya mdau wetu hiyo ni ''KWA TAARIFA YAKO'' hii leo kama ulikuwa hujui, vinginevyo tukutane wiki ijayo au wasiliana nasi kwa barua pepe gospelkitaa@post.com. BARIKIWA